Umoja wa Upinzani Kenya Kumtangaza Atakayepeperusha Bendera Aprili 27, 2017.

No comments

Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA umesema kuwa utamtangaza atakayeshikilia bendera yake ya urais mnamo tarehe 27 mwezi Aprili 2017.

Akizungumza katika mkutano wa kumlaki gavana wa kaunti ya Bomet Isack Ruto kujiunga na muungano huo kama mmoja wa viongozi wakuu wa chama hicho, waziri wa zamani wa maswala ya kigeni ambaye pia ni seneta wa kaunti ya Bungoma Moses Wetangula amesema kuwa kiongozi huyo atatajwa katika mkutano utakaofanyika uwanja wa Uhuru Park uliopo katikati ya jiji la Nairobi.

Amesema kwamba tayari viongozi hao ambao wamekuwa wakikutana kwa takriban siku tatu zilizopita wamepiga hatua ya kumchagua mmoja wao kuongoza muungano huo.

Viongozi wakuu wa muungano wa NASA ni aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga wa chama cha ODM, aliyekuwa wakati mmoja makamu wa rais Kalonzo Musyoka, wa chama cha Wiper, Moses Wetangula wa chama cha Ford Kenya na Issack Ruto wa chama cha mashinani CCM.

Awali akizungumza katika mkutano huo aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga alisema kuwa chama hicho sasa kitakuwa na baraza kuu kwa jina ”NASA Pentagon” kufuatia kujiunga kwa Issack Ruto.
Viongozi wote wakuu wa muungano huo walihudhuria mkutano huo katika ukumbi wa Bomas of Kenya Jijini Nairobi.

No Comments Yet.

Leave a comment