Sakata la kadi tatu za njano lavaa sura Mpya

No comments

Sakata la kadi tatu za njano linalomuandama mchezaji wa Kagera Sugar Mohamed Faki, limewavaa mashabiki na wanachama wa klabu za Simba na Young Africans huku saa kadhaa zikisalia kabla ya kamati ya saa 72 haijatangaza maamuzi ya rufaa iliyowasilishwa mezani kwao na viongozi wa Wekundu wa Msimbazi.

Kipindi cha Wizara ya Michezo kupitia Redio Times Fm 100.5 kimefanya mahojiano na baadhi ya mashabiki wa klabu ya hizo mbili, kufuatia kauli nzito iliyoptolewa jana na mjumbe wa kamati ya utendaji ya Young Africans Salum Mkemi kwa niamba na viongozi wenzake.

Hassan Salum mwanachama wa klabu ya Simba kutoka Tawi la Ubungo Terminal amesema ameshangazwa na kauli iliyotolewa jana na Mkemi kwa kusema hawatokubali maamuzi ya kamati ya saa 72 endapo itaondoa alama tatu kwa Kagera Sugar.

Kwa upande wa Baadhi ya mashabiki wa Young Africans wamesema wanaungana na uongozi wao kupitia kauli iliyotolewa jana na Salum Mkemi, huku wakionyesha bado wana matumaini makubwa ya kikosi chao kutetea ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2016/17.

Sintofahamu ya rufaa ya klabu ya Simba dhidi ya Kagera imevuka bahari hadi visiwani Zanzibar ambapo mwanachama na shabiki wa Young Africans tawi la Mwanakwerekwe Meli Nne Mohammed Hassan Papao maarufu kama Jerry Muro, ameujia juu uongozi wa TFF kutokana na sakata la rufaa ya Simba dhidi ya mchezaji wa Kagera Sugar.

Akizungumza na kipindi Cha Wizara ya Michezo kwa njia ya simu  kutoka kisiwani Unguja Papao amesema kuna mizengwe ambayo inapangwa na TFF kuhusiana na suala hilo.

Shabiki huyo ambaye mavazi yake yote mpaka kofia ya Msikiti ina rangi na nembo za Yanga, amesema anapata hofu kutokana na kamati ya saa 72 kutangaza baadhi ya maamuzi waliyoyachukua, lakini wakaliacha sakata la rufaa ya Simba dhidi ya Kagera Sugar.

No Comments Yet.

Leave a comment