klabu ya Simba SC imetoa kauli kuhusu,sakata la kadi tatu za njano.

No comments

Baada ya kukaa kimya kuhusu sakata la kadi tatu za njano linalomuhusu mchezaji wa Kagera Sugar Mohamed Fakhi, uongozi wa klabu ya Simba SC hii leo umeibuka na kutoa kauli nzito huku wakijibu baadhi ya maneno yaliyowahi kutolewa na watani zao wa jadi Young Africans, kupitia mikutano na waandishi wa habari.

Simba SC hawajawahi kuzungumza lolote tangu walipopewa point tatu na mabao matatu na kamati ya saa 72 juma lililopita, hali ambayo ilidhaniwa huenda upande wa Msimbazi usingejishughulisha na sakata hilo ambalo limeibuliwa tena na uongozi wa Kagera Sugar, kwa kuitaka kamati ya sheria, Katiba na hadhi za wachezaji kutoa tafsiri ya kisheria kuhusu maamuzi yaliyopelekea wapokwe point tatu na mabao matatu.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano klabu ya Simba SC, Haji Manara leo amezungumza na vyombo vya habari makao makuu ya klabu hiyo (Mtaa Wa Msimbazi) na amesema hawatishwi na wapinzani wao waliosema wanamwaga mboga kuhusiana na kupewa pointi 3 dhidi ya Kagera Sugar na sasa kama vipi wao watabutua sahani na bakuli wakose wote.

Kauli hiyo ya Manara imekuja kufuatia kuwepo sintofahamu juu ya pointi 3 walizopewa na kamati ya saa 72, huku akisema anashangazwa na watani wao wa jadi kushikia bango suala hilo ili hali likiwa haliwahusu.

Manara amesema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari Makao Makuu ya klabu ya Simba, kuhusiana na hali inavyoendelea kuhusiana na Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji, TFF na Simba juu ya maamuzi ya Kamati ya saa 72.

“Juzi kiongozi mmoja wa Yanga ameongea na vyombo vya habari na kuitishia TFF kwamba wameenda TAKUKURU na Polisi kuomba wafanya uchunguzi juu ya maamuzi ya kamati ya saa 72, baadae TFF wanaitisha kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji kupitia maamuzi yaliyotolewa na kamati ya saa 72” amesema Manara.

Huo mkwara wa Yanga umewatisha sana TFF, sasa na sie Simba tunasema kama wao wamemwaga mboga, na sie tunabutua sahani na bakuli tukose wote, sababu TFF inaonekana kuipendelea Yanga kwa kila jambo.

Aidha Manara amesema, Nani asiyejua Kamati hiyo ya Sheria na wachezaji mpaka leo haijatoa maamuzi juu ya suala ya Tambwe dhidi ya Juuko? mwaka wa pili unamalizika,  Banda kampika ngumi Kavilla ndani ya wiki moja uamuzi umeshatolewa, hii kamati tunashindwa kuielewa?

Kagera kukata rufaa dhidi ya Simba ndani ya wiki wameshakaa kikao kupitia taarifa, nasema hivi sisi watoto wa mjini hatuwezi kukubali TFF kuwa inawabeba upande mmoja tu.

Tunawapa mpaka kufikia jumatatu tarehe 24 Machi, TFF wawe wametoa maamuzi juu ya kesi mbalimbali zilizopo kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, vinginevyo hatutakubali, tutabutu sahan tukose wote.

No Comments Yet.

Leave a comment