Kauli ya waziri yakanushwa

No comments

WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, imesema haijatoa waraka wowote unaowataka wanafunzi wote kusoma masomo ya sayansi badala yake imekuwa ikihamasisha wanafunzi kuchukua masomo hayo.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Stella Manyanya, alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Susan Lyimo.

Lyimo alitaka kujua Waziri alipata wapi mamlaka ya kutangaza kuwa vijana wote wa elimu ya msingi hadi kidato cha nne kusoma masomo yote ya sayansi.

“Je, kuna utafiti gani uliofanyika na matokeo kuonyesha haja ya vijana wote kusoma sayansi yaani Kemia na Fizikia?” Alihoji.

Akijibu swali hilo, Manyanya alisema Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1995 inampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya elimu kutangaza jambo lolote kwa maslahi ya taifa.

“Kuna haja kubwa ya kuhamasisha ongezeko la wanasayansi kulingana na hali halisi ya mahitaji, mfano kuna upungufu wa walimu wa sayansi na hisabati 24,716,” alisema.

Pia alibainisha kuna upungufu wa walimu 355 wa masomo ya ufundi katika shule za sekondari za ufundi na mafundi sanifu wa maabara za shule takribani 10,000.

“Moja ya majukumu ya Waziri ni kuhamasisha wanafunzi katika elimu ikiwa ni pamoja na kuchukua masomo ya sayansi, kuna taarifa mbalimbali zikiwamo za kimazingira halisi zinathibitisha juu ya upungufu wa wataalamu wa sayansi,” alisema.

Aidha alitolea mfano upande wa sekta ya Afya ili kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua inatakiwa akina mama hao wahudumiwe na matabibu wenye ujuzi, lakini hawapo wa kutosha.

Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Kuteuliwa, Anne Kilango, alihoji kama serikali haioni kuwa kujikita kwenye ubobezi ni muhimu kuliko kulazimisha watoto wasome sayansi.

Akijibu swali hilo, Manyanya alisema mchepuo huanza na msingi na nchi inahitaji wataalamu tofauti tofauti ambao wengine ni wabobezi ambao wamejikita eneo moja na wanahitajika wanaokuwa kimapana ambao wataweza kuoanisha pande mbili.

#Nipashe

No Comments Yet.

Leave a comment